Monday, March 14, 2011

DAR YAPOKEA Sh 147mil ZA WAATHIRIKA WA MAKOMBORA

OFISI ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam,imepokea zaidi ya Sh147 milioni, zikiwa ni msaada kwa watu walioathiriwa na milipuko ya makombora ya katika Kikosi cha 511 KJ cha JWTZ Gongo la Mboto.
Fedha hizo zimetokana na michango ya makundi mbalimbali ya wahisani, waliojitolea kuwasaidia wananchi walioathiriwa na milipuko hiyo iliyotokea usiku wa Februari 16 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, wakati akipokea taarifa kuhusu nyumba zilizofanyiwa uhakiki baada ya kuharibiwa kwa milipoko,Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki alisema makundi mbalimbali ya wananchi yamejitolea kutoa misaada ya fedha kwa ajili ya watu walioathiriwa.
Kwa mujibu wa Sadiki, sehemu ya fedha hizo zilikuwa taslimu na nyingine zilikuwa zimewasilishwa kwa njia ya hundi."Tumepokea Sh147 milioni kutoka kwa wahisani mbalimbali nchini ambao kwa namna moja au nyingine, wamejitolea kuwasaidia waathirika wa mabomu, lengo ni kuonyesha ushirikiano wao na kuguswa kwa tatizo hilo," alisema Sadiki.
Alisema fedha zingine ambazo hazimo katika hesabu hizo, zimekabidhiwa katika Ofisi ya Waziri mkuu (Kitengo cha Maafa) na kwamba taarifa zake zitatolewa hivi karibuni.
Kwa mujibu Sadiki, bado misaada inaendelea kutolewa sababu waathirika wanahitaji kusaidiwa hadi watakapopata makazi ya kudumu.Aliwasihi wananchi wanaoguswa na maafa yaliyowakumba wananchi, wanapaswa wajitolee kwa hali na mali kuwasaidia.
Alisema,tathimini ya awali imeonyesha kuwa, zaidi ya nyumba 3,000 zimepitiwa na watalaam wa tathmini na zaidi ya nyumba 79 zimeharibiwa kwa mabomu.Mkuu huyo wa mkoa Alisema, kwa takwimu hizo, zaidi ya familia 1,000 zinahitaji misaada inayojumuisha vyakula, mahema na mahitaji mengineyo.
Milipuko ya makombora katika Kikosi cha 511 KJ Gongo la Mboto, ilisababisha zaidi ya watu 20 kupeteza maisha na wengine mamia, kujeruhiwa.Hali kadhalika, ilisababisha uharibifu mkubwa wa makazi ya watu ambao sasa wamebakiwa wakiwa hawana mahali pa kuishi.

No comments: