Friday, March 11, 2011

USIHIFADHI MOYOWAKO PASIPO NA MAPENZI YA DHATI-2

NINA furaha sana kukutana nanyi tena katika ukusara wetu wa kupeana mawili matatu juu ya haya maisha yetu ya kiuhusiano. Bila shaka upo tayari kupokea kitu kipya kichwani mwako ambacho kitakuwa silaha yako ya kukulinda katika ulimwengu wa mapenzi.

Rafiki zangu, kitabu changu kipya cha Let’s Talk About Love kinapatikana mitaani sasa. Ndani ya kitabu hicho utakutana na mada nzuri za uhusiano pamoja na ‘Love Messages’ kali kwa ajili ya kutia nakshi penzi lako. Ni suluhisho katika ndoa, uhusiano na penzi lako. Hakikisha hukikosi.

Mada iliyopo mezani ni juu ya kuchunguza kama mwenzi uliyenaye ana mapenzi ya dhati au hana. Lengo hasa ni kuangalia kama moyo wako umeuhifadhi kwenye kiota cha huba ya kweli au kwenye mbigiri zenye kutoboa na kukuacha na maumivu makali.


Ndugu zangu, mapenzi hayapo kwa ajili ya kututesa na kutuumiza, ni kwa ajili ya kutupatia furaha maishani. Unajua mtu ambaye hana mpenzi mwenye mapenzi ya kweli, anayeelewana naye, lazima atakuwa na matatizo kuanzia ya kiafya mpaka ya utendaji wa kazi zake.

Ukiwa na mwenzi sahihi, ni rahisi hata kupanga mipango yako na kwenda sawasawa, maana kichwani mwako huna ‘stress’ za kukusumbua. Umenipata rafiki?

Sasa hebu tuendelee na vipengele vingine, tuweze kuona mwenzi uliyenaye ni sahihi au umehifadhi moyo wako kwenye moto? Twende tukaone.

HAYUPO HURU
Mpenzi wa aina hii, atakuwa na ‘nakupenda nyingi’ sana mdomoni mwake, lakini hayupo huru kabisa kwako! Siku zote huwa mnakutana chumbani tu, hata kama siyo chumbani labda mmepanga kutoka basi mtakutana huko huko!

Hapendi kuongozana na wewe na huwa na visingizio kibao.
Anaweza kukuambia mkutane mahali fulani na kama ukipendekeza muongozane atakataa na kukupa visingizio visivyo na msingi.

Mbaya zaidi mnaweza kuwa pamoja na mkaamua kwenda mahali fulani, bado atang’ang’ania utangulie hatua kadhaa au yeye atangulie halafu wewe ufuate nyuma! Kwanini? Huwezi kujiuliza hapo na ukapata jibu la wazi kabisa?

Kuna tatizo, anaona hana hadhi ya kuwa na wewe, anakudharau lakini anashindwa kuachana na wewe kwa sababu ana mambo yake anayoyapata kutoka kwako. Hapo unapaswa kuzinduka, kuchekecha ubongo wako na kuchukua hatua.

Kama anakupenda kwa nini anashindwa kuongozana na wewe, kwa nini anakataa msiwe pamoja kwenye hadhara, anamwogopa nani kama siyo hakupendi? Fikiria zaidi!

HAKUSHIRIKISHI...
Mpenzi wa aina hii, hashindwi kukuambia anakupenda wakati mwingine hata mara tatu au zaidi kwa siku lakini kamwe hakushirikishi katika mambo yake. Hataki kukuambia na anaonesha wazi wazi kuwa hapendi kukushirikisha.

Hata kama utaonesha dalili za kutaka kujua mambo yake na kumsaidia mawazo, hataonesha kufurahia jambo hilo, mara nyingi anataka kufanya mambo yake kwa kificho bila kuingiliwa maamuzi yake.

Utakapohitaji kumsaidia, atakuambia mambo yanayomhusu yeye umuachie mwenyewe. Hili ni tatizo tunapozunguzia mapenzi ya dhati. Wapenzi siku zote hushirikiana. Kama hataki kukushirikisha, kuna maana gani yeye kuendelea kukuimbia wimbo wa ‘nakupenda’ kila wakati?

HAZUNGUMZII MAHABA
Kipengele hiki kinahusu mambo ya chumbani zaidi! Mpenzi wa aina hii kama hutamkumbusha wewe basi mnaweza kumaliza hata mwezi mzima bila kukutana kimwili.

Hujifanya mchovu au mwenye mambo mengi, hayo yote siyo ya kweli, hukwepa kufanya mapenzi na wewe kwa sababu hana msisimko kwako. Inawezekana ameshakuchoka lakini anashindwa kukuambia ukweli, anakuacha uangalie mwenyewe mambo yake na ikiwezekana uchukue hatua!

Hivi unafikiri ni mpenzi gani mwenye mshawasha na mwezake atakayeweza kukaa mwezi mzima bila kukutana kimwili na patna wake? Hakika haiwezekani. Mwenzi anapokuwa katika hatua hii, jua tu ameshaanza kukuchoka au ana mpenzi mwingine nje anayemchengua.

Naomba nisieleweke vibaya katika kipengele hiki, kwanza hakuna maana kwamba kufanya ngono ndiyo mapenzi au kukutana kimwili ndiyo uthibitisho wa mapenzi ya kweli, lakini kwa wenzi ambao tayari wameshaanza kukutana chumbani kipengele hiki kinawahusu sana.

Haiwezekani ratiba ibadilike ghafla, wakati mwanzoni yeye ndiyo alikuwa msumbufu akikuhitaji faragha. Hii alama ya kukuchoka, kukukinai au kuwa amepata mwingine ambaye anamudu zaidi yako. Upo hapo?

KWA NINI UUTESE MOYO WAKO?
Kukuambia anakupenda kila wakati hakuwezi kukuthibitishia kuwa ana mapenzi ya kweli ikiwa kuna kasoro nilizoanisha hapo juu. Ikiwa kasoro zote zipo na ukafanya uchunguzi na kugundua kuwa mwenzi uliyenaye hakupendi, usiteseke zaidi!

Chukua hatua, epusha matatizo katika moyo wako, upe haki ya kuwa na furaha, unapaswa kufurahia mapenzi na siyo kutesekea mapenzi! Katika hali kama hiyo, nakuachia maamuzi mwenyewe.

Ikiwa una maswali zaidi, unahitaji ufafanuzi wa namna ya kufurahia mapenzi au mambo mengine zaidi juu ya uhusiano tafadhali wasiliana nami ila usibipu! Mada imeisha, karibuni tena wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri zaidi. Naweka nukta.

No comments: