Tuesday, March 5, 2013

UHURU KENYATTA BADO AONGOZA MATOKEO YA AWALI

Naibu Waziri Mkuu wa Kenya Uhuru Kenyatta


Uhuru Kenyatta mgombea kiti cha urais nchini kenya anayekabiliwa na mashitaka ya kimataifa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu , bado anaongoza kwa kiasi kikubwa katika upigaji kura katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.

Huku kukiwa karibu nusu ya kura zimehasibiwa matokeo yasiyo rasmi yanaonyesha Bw.Kenyatta akiongoza dhidi ya mpinzani wake mkuu Raila Odinga  kwa asilimia 53 dhidi ya 43. Maafisa wanasema wanatarajia matokeo kamili  Jumatano.

Maafisa wa uchaguzi wanasema karibu kura laki tatu na thelathini zimekataliwa mpaka sasa kwa kutokufuata taratibu za upigaji kura. Huku mshindi akitakiwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa , baadhi ya wachambuzi wanabashiri kwamba Bw.Kenyatta atashindwa kupata ushindi wa eneo zima na kukumbana na duru ya pili.

Bw.Kenyatta mtoto wa rais wa kwanza wa Kenya na mmoja wa watu matajiri sana barani Afrika , anakabiliwa na mashitaka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa shutuma za kupeleka vikosi vya mauaji ambavyo vilifanya mashambulizi ya kuwaadhibu  wafuasi wa upinzani baada ya uchaguzi uliopingwa wa mwaka 2007.
Watu wakijipanga msululu kwenda kupiga kura

No comments: